Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atangaza Kupumzika Ubunge

-rickmedia: Lanka Ting

Lanka Ting

2 days ago
rickmedia: waziri-mkuu-kassim-majaliwa-atangaza-kupumzika-ubunge-787-rickmedia

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametangaza rasmi kustaafu kugombea tena Ubunge wa Jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi, baada ya kuliongoza kwa takribani miaka 15 mfululizo tangu mwaka 2010.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka kwa wandani wa Waziri Mkuu Majaliwa vimeieleza Jambo TV kuwa, akiwa jimboni kwake Ruangwa kwa siku kadhaa za mashauriano na wananchi na wazee wa eneo hilo, Majaliwa amefikia uamuzi huo baada ya tafakari ya kina na ushauri wa wadau mbalimbali na amewashukuru Wanaruangwa kwa kipindi chote cha miaka 15 ya kumpa ubunge na kuwawakilisha vyema.

Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya Majaliwa kutangaza Bungeni, Juni 26, 2025, kuwa anapanga kugombea tena ubunge wa jimbo hilo, akisisitiza kuwa anaendelea kuhitaji ridhaa ya wananchi. Hata hivyo, kauli hiyo sasa imebadilika rasmi.

"Ninatambua wakati mwingi nimekuwa nje ya jimbo nikilitumikia taifa lakini wana Ruangwa wameendelea kuniunga mkono. Nitumie nafasi hii kusema asanteni sana na ninamuomba Mwenyezimungu azidi kuimarisha mshikamano uliopo kati yetu sote. Ninaomba kuwajulisha kuwa ninakuja kuchukua fomu ya kuomba ridhaa yenu tena.", alinukuliwa bungeni.

Uamuzi wa Majaliwa umepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya wachambuzi wa siasa wakiutaja kuwa ni uamuzi wa busara na wa kiungwana, hasa baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka 10 cha Uwaziri Mkuu tangu alipoteuliwa mwaka 2015.

Hatua hii pia inakuja wakati chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa katika harakati za ndani za uteuzi wa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Zoezi hilo limeanza Juni 28 na linatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025.