Pacome Zouzoua na Clement Mzize wamekuwa mashujaa wa Yanga leo hii baada ya kuiongoza timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yaliyoihakikisha timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Matokeo hayo yameifanya Yanga imalize ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi na pointi 82 huku Simba ilimaliza katika nafasi ya pili na pointi 78.
Zouzoua alitangulia kuifungia Yanga katika dakika ya 66 kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na refa Mohamed Amin baada ya kipa Moussa Camara kumfanyia faulo kiungo huyo wa Yanga katika eneo la hatari.
Wakati Simba ikipambana kusaka bao la kusawazisha, Mzize ambaye aliingia uwanjani akitokea benchi, aliipatia Yanga bao lililozika rasmi matumaini ya Simba kupata ushindi na kutwaa ubingwa akimalizia vyema pasi ya Pacome.
Ushindi huo haukupatikana kwa kubahatisha kwa Yanga kwani ilionekana kutawala muda mwingi wa mechi ikitengeneza nafasi nyingi tofauti na Simba ambayo ilifanya hivyo mara chache huku ikitengeneza idadi ndogo ya nafasi.