Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amedai kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki na taratibu za uchaguzi siku ya kupiga kura, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini humo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Bobi Wine amesema huduma ya intaneti imezimwa makusudi siku ya uchaguzi, jambo linalodhoofisha mawasiliano na uwazi wa mchakato mzima wa kidemokrasia. Aidha, amedai kuwa kumekuwepo na matukio mengi ya kujazwa kura kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa upinzani, baadhi ya viongozi wa chama chake, akiwemo Naibu Rais wa Kanda ya Magharibi, wamekamatwa na vyombo vya dola. Vilevile, mawakala na wasimamizi wengi wa uchaguzi wanadaiwa kutekwa nyara, huku wengine wakifukuzwa katika vituo vya kupigia kura, hali inayotilia shaka uhalali wa zoezi hilo.
Bobi Wine pia amesema mashine za utambuzi wa wapiga kura (BVVK) zimeshindwa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.