Mahakama ya Rufaa ya Marekani imeidhinisha uamuzi wa jopo la majaji kwamba Rais wa Marekani Donald Trump alipe fidia ya dola milioni 83.3 kwa mwandishi E. Jean Carroll kwa kumdhalilisha hadharani kupitia mitandao ya kijamii na matamshi ya umma. Mahakama hiyo imesema kuwa uharibifu alioupata Carroll kutokana na matamshi ya Trump ulikuwa mkubwa na wa kipekee, ukizingatia vitisho vya kuuawa alivyopokea.
Trump alikuwa ameomba kesi hiyo isikilizwe upya, akidai fidia hiyo ni kubwa kupita kiasi, lakini ombi lake lilikataliwa. Mahakama imesisitiza kuwa Trump alionyesha dharau kubwa kwa usalama na afya ya Carroll kwa kuendelea kumshambulia hadharani kwa miaka mitano, hata wakati wa kesi ikiendelea.
Tukio la awali lilidaiwa kutokea mwaka 1996 ambapo Carroll alidai kushambuliwa kingono na Trump katika duka la Bergdorf Goodman jijini New York. Trump alikana madai hayo na kusema Carroll si "aina yake." Kesi hii sasa huenda ikapelekwa Mahakama ya Juu ya Marekani.