Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Sefu Shabani ‘Matonya’, leo Alhamisi Aprili 9, 2026 amefikishwa mahakamani katika eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa nchini Kenya, akikabiliwa na shtaka la ubakaji.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa Aprili 7, 2026, katika jengo la Josy Joka Apartments lililopo Nyali, Mombasa, msanii huyo anadaiwa kumuingilia kimwili mwanamke aliyetajwa katika nyaraka za mahakama kwa herufi J.G, kwa kutumia nguvu.
Matonya, anayefahamika zaidi kupitia wimbo wake maarufu “Vaileti”, ameshtakiwa kwa kosa hilo chini ya Kifungu cha 3(1)(a) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Makosa ya Kingono nchini Kenya.
Mbali na shtaka hilo kuu, msanii huyo pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kufanya kitendo kisichofaa kwa mtu mzima, ambapo mahakama iliambiwa kuwa alimgusa mwanamke huyo katika sehemu zake za siri bila ridhaa yake.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, mahakama ilimruhusu mshtakiwa kupewa dhamana ya Shilingi 500,000 za Kenya, sawa na takriban Shilingi milioni 10 za Tanzania, kwa sharti la kuwa na mdhamini mmoja raia wa Kenya mwenye dhamana ya kiasi kama hicho.