Mzee wa miaka 82 amuua mwanaye wakigombania koti

-rickmedia: Saraphina Jerry

Saraphina Jerry

3 days ago
rickmedia: mzee-miaka-amuua-mwanaye-wakigombania-koti-262-rickmedia

Mzee mwenye umri wa miaka 82, mkazi wa kijiji cha Kilema, kata ya Olele, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kumuua na kumzika mwanaye, Oscar Msamanga (42), kufuatia ugomvi uliodaiwa kuzuka baada ya Msamanga kuvaa koti la baba yake bila idhini.

Tukio hilo la kusikitisha lilifichuka Aprili 29, 2025, baada ya mzee huyo kutoa kauli ya kushtua hadharani wakati wa sherehe kijijini, akidai kuwa alimuua mwanaye na tayari alikuwa amemzika kwenye shimo alilolichimba pembeni mwa nyumba yao.

Mwandishi wa habari hii, alifika katika eneo la tukio na kushuhudia polisi wakifukua mwili wa marehemu, ambapo baada ya kufukuliwa ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Karume kwa ajili ya taratibu za uchunguzi zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa mauaji hayo yalitokea Aprili 27, huku mwili wa marehemu ukigundulika Aprili 29 na kufukuliwa Aprili 30 baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.

"Ni kweli tukio hili limetokea katika Kijiji cha Kilema, Mzee huyu na marehemu walikuwa wakiishi pamoja na walikuwa na mgogoro, inadaiwa kuwa chanzo cha tukio ni kitendo cha kijana huyo kuvaa koti la baba yake, jambo lililomghadhabisha mzee huyo," amesema Kamanda Maigwa.