Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, linawashikilia watuhumiwa wawili (majina yao yamehifadhiwa kwa uchunguzi) kwa kosa la kumlawiti na kisha kumuua mtoto Christina Shabani mwenye umri wa miaka 7.
Tukio hilo limetokea Oktoba 15, 2026 saa 11 jioni huko mtaa wa Ikulu Kata ya Kawajense Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, ambapo watuhumiwa walimvizia marehemu akiwa peke yake anacheza umbali kidogo na nyumbani na kisha kumfanyia unyama huo.
Mahojiano ya kina na watuhumiwa hawa bado yanaendelea na mara baada ya kukamilika taratibu nyingine za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linasikitishwa sana na tukio la mauaji ya mtoto lililotokea na linatoa pole nyingi kwa familia, ndugu na jamii yote, pia linawasihi wananchi kutofumbia macho vitendo viovu vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia bali waripoti kwa Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati kabla madhara kutokea.