JOHANNESBURG – Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa kundi la pili la raia wake waliokuwa wameingizwa kwenye mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine kuipigania Urusi, linatarajiwa kurejea nyumbani hivi karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne hii, ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa imethibitisha kuwa wanaume 11 kati ya kundi la watu 17 waliokuwa wamekwama vitani wako njiani kurejea. Hatua hii inakuja baada ya watu wanne wa kwanza kuwasili nchini humo wiki iliyopita.

Suala la vijana hao 17 lilichukua sura mpya mwezi huu baada ya Rais Ramaphosa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa njia ya simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Vijana hao walikuwa wametuma ujumbe wa kuomba msaada mnamo Novemba mwaka jana baada ya kujipata wamenaswa katika jimbo la Donbas, Ukraine, wakidai walihamasishwa kwenda Urusi kwa ahadi za kazi lakini badala yake wakapelekwa mstari wa mbele wa mapambano.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo:
- Watu 11 wanarejea nchini hivi karibuni.
- Watu 2 bado wako nchini Urusi, mmoja akiwa amelazwa hospitalini jijini Moscow.
- Watu 4 tayari walishawasili Afrika Kusini wiki iliyopita.
Mgogoro wa Ajira na Utumwa wa Kivita
Ripoti za raia kutoka mataifa ya Afrika kushawishiwa kwenda Urusi kwa ahadi za ajira nono na kisha kuishia vitani zimeongezeka hivi karibuni, jambo linalozua mivutano ya kidiplomasia kati ya Moscow na washirika wake barani Afrika.
Wiki iliyopita, ripoti ya idara ya usalama ya Kenya iliyowasilishwa bungeni ilikadiria kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 wameajiriwa kupigana upande wa Urusi nchini Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya amepanga kuzuru Urusi hivi karibuni kushughulikia suala hilo.
Msimamo wa Afrika Kusini
Afrika Kusini imekuwa ikijaribu kulinda msimamo wake wa "kutofungamana na upande wowote" katika mgogoro wa Ukraine, huku ikidumisha uhusiano wa karibu na Moscow kupitia umoja wa BRICS. Hata hivyo, kashfa hii ya raia wake kuingizwa vitani inatajwa kuweka msimamo huo kwenye mtihani mgumu.